Tanzania



HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR DK. ALI MOHAMED SHEIN KATIKA SHEREHE ZA MIAKA 48 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR, TAREHE 12 JANUARI 2012.Assalaam Alaykum,Ndugu Wananchi;Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma, Aliyetakasika, kwa kutujaaliya kufika siku hii ya leo kuadhimisha miaka 48 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, tukiwa wenye afya njema, amani, mshikamano, umoja na furaha. Pamoja na kuadhimisha mwaka wa 48 wa Mapinduzi pia tumekamilisha mwaka mmoja tangu kuanza kwa Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa.Wakati tunasherehekea miaka 48 ya Mapinduzi, tuna wajibu mkubwa wa kuwakumbuka viongozi wetu, waasisi wa Mapinduzi walio hai na waliotangulia mbele ya haki. Tunaomba Mola wetu Karimu awape wote hao rehema zake. Jasho na juhudi zao ndio zimetufikisha hapa tulipo leo. Nchi yetu ipo shwari, tulivu na ina amani.Ndugu Wananchi,Natoa shukurani kwenu viongozi mbali mbali, wananchi, wageni wetu mbali mbali, kwa kuhudhuria sherehe hizi muhimu katika historia ya nchi yetu. Natoa shukurani za dhati kwenu nyote kwa kujumuika nasi kwenye maadhimisho haya.Aidha, natumia fursa hii kukupongezeni Watanzania nyote kwa kuadhimisha kwa amani, salama na mafanikio makubwa miaka 50 tangu Tanzania Bara ipate uhuru. Maadhimisho hayo yaliyofikia kilele chake mwezi uliopita, yalitowa tathmini ya maendeleo ya Watanzania kwenye sekta zote. Kwa hakika sote tumefarajika kwa hatua kubwa ya maendeleo iliyofikiwa chini ya uongozi wa awamu zote nne za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kipindi hiki cha miaka 50.Ndugu Wananchi,Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 yamezaa matunda mema yaliyotokana na ahadi za ASP chini ya Uongozi wa Jemedari wetu wa Mapinduzi, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, tangu wakati wa kupigania uhuru. Miongoni mwa matunda yaliyopatikana ni kuurejesha utu na heshima ya wanyonge, kuondoa aina zote za ubaguzi, ardhi yote kuwa mali ya Serikali, kuifanya elimu kuwa bila ya malipo kwa wananchi wote, kufanya matibabu kuwa bure kwa wote bila ya ubaguzi, kuimarisha makaazi ya wananchi na kuwapatia wazee na wasiojiweza makaazi na msaada maalumu wa kuendesha maisha yao.Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, kama ilivyokuwa kwa awamu nyengine sita zilizopita, inayaendeleza kwa vitendo malengo hayo, kwa kuhakikisha kuwa uchumi wetu unaendelea kustawi na huduma za jamii zinaimarishwa na kuwafikia wananchi wote wa Unguja na Pemba, bila ya ubaguzi wa aina yoyote.Ndugu Wananchi,Maendeleo endelevu yanaanzia kwa kuwepo mipango mizuri inayozingatia mabadiliko ya wakati na yenye kusimamiwa na taasisi zenye uwezo. Kwa upande wetu, Serikali imeendelea na hatua za kuimarisha mfumo wa kitaasisi pamoja na kuufanyia mapitio Mpango wetu mkuu wa Maendeleo, yaani Dira ya Maendeleo ya hadi mwaka 2020. Juhudi za kuiunda upya Tume yetu ya Mipango zilizoanza mwaka jana, bado zinaendelea. Tunaupitia upya Muundo wa Tume hiyo sambamba na kuipitia Sheria Namba 5 ya mwaka 1989 iliyoianzisha. Tunatarajia kuwa tutawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hiyo katika kikao cha mwezi wa Aprili cha Baraza la Wawakilishi, ili kuimarisha zaidi kazi za Mipango Serikalini. Kwa upande mwengine, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo iko katika hatua za mwisho za mapitio ya Dira ya 2020 na inatarajiwa kwamba taarifa ya mwisho itawasilishwa rasmi Serikalini hivi karibuni. Juhudi hizi zote zinazofanywa na serikali ni katika kuweka programu muhimu za maendeleo zitakazozalisha kazi zenye tija na heshima kwa wananchi wake. Aidha, jitihada hizi zitajenga misingi madhubuti ya uwekezaji na kuongeza pato la taifa.Ndugu Wananchi,Mfumo wa dunia yetu hivi sasa umekuwa ni wa kutegemeana zaidi, kwani dunia imekuwa kama kijiji kutokana na utandawazi na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano. Athari za kiuchumi zinazotokea katika sehemu moja ya dunia, zinaathiri sehemu nyingine. Kwa hivyo, juhudi za kuimarisha uchumi wetu zimekuwa kwa kiasi fulani zikiguswa na matukio ya ulimwenguni kama vile mtikisiko wa uchumi, kupanda kwa bei za mafuta na chakula, misukosuko ya kisiasa, uhaba wa mvua na uharibifu wa mazingira pamoja na harakati za uharamia katika Bahari ya Hindi. Sababu zote hizo zinaathiri uchumi wa dunia kwa kiasi kikubwa husababisha kupungua uzalishaji na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma mara kwa mara.Kwa upande wetu, Serikali inachukua juhudi mbali mbali za kuendeleza uchumi na ustawi wa wananchi wake. Kwa jumla, uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma hutegemea sana uimara wa vyanzo kama vile teknolojia, maliasili, maendeleo ya rasilimali watu na uwekezaji. Kwa mwaka 2010 kasi ya ukuaji halisi wa uchumi imefikia asilimia 6.5 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.7 mwaka 2009. Hali hii imetokana na ukuaji mdogo wa sekta za viwanda na huduma ambapo kwa mwaka 2010 ukuaji wa sekta ya huduma ulifikia asilimia 8.7 ikilinganishwa na asilimia 8.8 ya mwaka 2009.Aidha, ukuaji wa sekta ya viwanda ulikuwa asilimia 1.9 mwaka 2010 kutoka asilimia 3.4 mwaka 2009. Hata hivyo, ukuaji wa sekta ya kilimo uliimarika na kufikia asilimia 4.6 mwaka 2010 ikilinganishwa na asilimia 4.4 mwaka 2009.Kwa mwaka 2011 mfumuko wa bei umekuwa na changamoto. Hii imetokana na kuwa Zanzibar inategemea zaidi uagiziaiji wa bidhaa muhimu ikiwemo nishati ya mafuta, bidhaa za chakula na nyenginezo. Kwa bahati mbaya bei za bidhaa zote hizo hazikuwa na utulivu kwa mwaka 2011 na hivyo kuathiri mwenendo wa bei hapa nchini. Kasi ya mfumuko wa bei kwa Zanzibar imeendelea kuongezeka kutoka asilimia 6.6 (kwa miezi ya Januari 2010 na 2011) hadi kufikia asilimia 18.7 (kwa miezi ya Novemba 2010 na 2011). Ongezeko hili linaathiri shughuli mbali mbali za kiuchumi na kijamii.Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kupunguza ushuru katika bidhaa za vyakula kama vile mchele, unga wa ngano na sukari kwa lengo la kuwasaidia wananchi ili waweze kujikimu na maisha. Aidha, Serikali imeendelea kuwapatia wakulima pembejeo na ushauri ili waweze kuzalisha zaidi, kwa lengo la kupunguza uagiziaji.Ndugu Wananchi,Juhudi nyengine zinazochukuliwa katika kupambana na mfumuko wa bei kwa upande wa vyakula, ni kama zifuatazo:-1. Kuendelea kuimarisha uzalishaji wa mazao mbali mbali ya chakula hasa mpunga, muhogo, ndizi, viazi vitamu, viazi vikuu, kunde, mtama na jamii mbali mbali za mboga kwa kupitia uwezeshaji wa kitalaamu kwa kutumia mbinu za kisasa za skuli za wakulima.2. Katika kipindi cha mwaka mmoja Januari, 2011 hadi Disemba, 2011, Serikali imeziwezesha jumla ya skuli mpya 540 za wakulima na wafugaji, katika shehia 90 za Unguja na Pemba na kufanya idadi ya skuli za wakulima zlizoimarishwa hadi sasa kufikia 14,799. Lengo ni kuziimarisha skuli za wakulima 1200 hadi kufikia mwezi wa Januari, 2012.3. Matokeo ya juhudi hizi ni kuongezeka kwa tija katika uzalishaji wa mazao haya yaliyoanzishwa katika skuli za wakulima. Tathmini ya tija iliyofanywa imeonesha kuwa ongezeko kwa mazao ya muhogo kutoka wastani wa tani 9.5 kwa hekta, kabla ya mafunzo hadi wastani wa tani 17.6 kwa hekta baada ya mafunzo. Aidha, ongezeko hili limeonekana katika zao la ndizi, ambapo tija imeongezeka kutoka wastani wa tani 9 kwa hekta kabla ya mafunzo, hadi tani 15 baada ya mafunzo.Kwa upande wa mpunga wa umwagiliaji ongezeko limeonekana kutoka wastani wa tani 3.5 kwa hekta kabla ya mafunzo hadi wastani wa tani 5 kwa hekta baada ya mafunzo na mpunga wa juu, ongezeko la tija limeonekana kutoka wastani tani 1.9 kwa hekta kabla ya mafunzo, hadi tani 5 kwa hekta, baada ya mafunzo.Serikali imedhamiria kuongeza idadi ya skuli hizi za wakulima, ili ongezeko la tija lichangie katika uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kupunguza mfumko wa bei ya vyakula.Sambamba na juhudi hizi za kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali kupitia sheria namba 5 ya uhakika wa chakula na Lishe ya Zanzibar ya mwaka 2011, itaanzisha maghala ya akiba ya chakula, ili ziweze kuchangia katika kupunguza mfumko wa bei, kwa kuongeza chakula kinachoingia katika soko wakati wa upungufu wa chakula. Hatua za awali za kuanzisha maghala haya tayari zimeshachukuliwa kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo.Pamoja na misukosuko iliyosababisha matatizo ya kiuchumi na kupanda kwa mfumko wa bei, pato letu la Taifa limekua kwa asilimia 5.6 mwaka 2010/2011. Kutokana na juhudi za kuimarisha uchumi wetu, mapato ya serikali yameendelea kuongezeka. Katika mwaka wa fedha uliopita (2010/2011) tulitarajia kukusanya mapato ya ndani ya T.Shs. 171.68 bilioni, ambapo ukusanyaji halisi ulikuwa T.Shs. 181.48 bilioni na hivyo kuvuka lengo letu kwa asilimia 6. Haya ni maendeleo mazuri ikizingatiwa kwamba katika kipindi kama hicho, mwaka 2009/2010 mapato yaliyokusanywa yalikuwa T.Shs. 146,200 milioni. Taasisi zetu zote mbili za ukusanyaji, yaani TRA na ZRB, zilivuka lengo. ZRB ilivuka lengo kwa asilimia moja (1%) na TRA ilivuka lengo kwa asilimia 10 (10%). Natoa pongezi kwa watendaji wote wa taasisi hizi kwa kufikia kiwango hicho cha utendaji kwa mwaka huo. Hongereni sana.Ndugu Wananchi,Ili kuendeleza misingi ya mafanikio ya uchumi wetu iliyowekwa na awamu zilizopita, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba, imeimarisha usimamizi wa fedha za umma zikiwemo hatua za udhibiti wa misamaha ya kodi, kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika sekta ya utalii pamoja na mashirika na taasisi mbali mbali za umma.Katika miezi sita ya awali ya mwaka huu wa fedha wa 2011/2012, mapato yetu yanayotokana na vianzio vya ndani yameongezeka kwa takriban asilimia ishirini na mbili (22%) kutoka TShs. 83.2 bilioni zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka 2010/11 na kufikia TShs. 101.6 bilioni.Kwa jumla, mapato kutoka nje yakichanganywa na akiba yetu wenyewe tunayokuwa nayo, yanaufanya uwezo wetu wa fedha kufikia TSh. 167.5 bilioni katika miezi sita hiyo. Kutokana na uwezo huo, tumemudu kutumia TSh. 157.2 bilioni kwa shughuli za kawaida na zile za maendeleo. Mchango wa fedha zetu za ndani katika matumizi hayo, ulifikia TSh. 103.0 bilioni. Lengo la Serikali ni kuimarisha zaidi ukusanyaji wake wa mapato ya ndani ili tuweze kujitegemea na kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.Kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato na kwa kutilia maanani mchango uliotolewa na watumishi wa Serikali, ambao kwa sasa wamestaafu, Serikali imeweka mkazo maalum katika kulipa viinua mgongo kwa wakati. Ninafuraha kukujuilisheni kwamba tumeweza kuwalipa wastaafu wote hadi wa mwezi wa Novemba, 2011 ambao fomu zao zimeshakaguliwa na kuthibitishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu. Jumla ya wastaafu 491 wamelipwa mafao yao ya T.Shs. 3.00 bilioni katika kipindi cha Julai hadi Novemba, 2011. Wastaafu wa Disemba, 2011 watalipwa ndani ya mwezi huu wa Januari, 2012.Ndugu Wananchi,Kuhusu uwekezaji, Serikali hivi sasa ipo katika hatua ya kuifanyia mapitio ya sera, sheria na kanuni za uwekezaji ili kutoa fursa na vivutio zaidi katika sekta zote za kiuchumi na kuifanya Zanzibar kuwa ni kivutio cha wawekezaji wa ndani na wa nje.Katika mwaka wa fedha 2010/2011, jumla ya miradi 51 imeidhinishwa katika sekta mbali mbali. Idadi hii ni sawa na asilimia 85 ya lengo la kuvutia uwekezaji ambapo makadirio yalikuwa ni kuidhinisha miradi 60. Aidha, katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Julai hadi Disemba 2011, jumla ya miradi 20 ya uwekezaji imeidhinishwa ambayo ni sawa na asilimia 80 ya lengo lililowekwa la miradi 25. Miradi yote hiyo itakapokamilika itaweza kuvutia mitaji yenye thamani ya kiasi cha US$ 256.86 milioni na inatarajia kuzalisha ajira zisizopungua 3,500 kwa vijana wetu.Natoa wito kwa wananchi wa Unguja na Pemba tuzipokee na tuzikubali sera za uwekezaji na sisi wenyewe tuwe washiriki wakubwa katika uwekezaji, ili tuweze kutoa mchango wetu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi nchini mwetu.Kwa kutambua umuhimu wa mchango wa sekta ya kilimo katika kujenga msingi wa uchumi wa kisasa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba itaendelea kuimarisha Mapinduzi ya Kilimo.Serikali imefanya jitihada kubwa katika uimarishaji wa kilimo cha umwagiliaji katika hekta 8,521 zilizokwishaimarishwa. Hadi sasa hekta 715 zinalimwa mpunga, 511 Unguja na 204 Pemba. Umeme tayari umefikishwa kwenye Bonde la Cheju lenye ukubwa wa ekari 3000 kwa ajili ya kusaidia umwagiliaji maji. Kadhalika, mfumo wa mtandao wa maji umeanza kuwekwa, ili bonde hili liweze kutoa tani 5,000 za mchele kwa msimu. Lengo ni kupunguza uagiziaji wa mchele kutoka nje.Katika kutekeleza azma yetu ya kufanikisha Mapinduzi ya Kilimo, mapema katika mwezi wa Mei, 2011, nilipokuwa natembelea mashamba ya kilimo cha mpunga ya Unguja na Pemba, niliahidi kuchukua hatua ya kuwasaidia wakulima kwa kuwapunguzia bei ya huduma za matrekta pamoja na pembejeo za kilimo, zikiwemo mbegu, dawa, mbolea, pamoja na huduma nyengine. Ahadi hiyo, ilitekelezwa kwa kuzipunguza bei za pembejeo za kilimo na huduma za matreketa kwa asilimia kati ya 50-75 na bei hizo zikatangazwa rasmi kwenye bajeti ya Wizara ya Kilimo na Maliasi katika mwezi wa Julai 2011. Aidha, idadi ya matrekta na vifaa vyengine vinavyofanikisha shughuli za kilimo imeongezwa ili kukidhi mahitaji ya wakulima nchini. Uzinduzi wa msimu wa kilimo wa mwaka 2011/2012 nilioufanya katika bonde la Cheju, nilishuhudia jinsi wakulima walivyofaidika na walivyohamasika na uamuzi huo wa Serikali.Ndugu Wananchi,Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili bado inaendelea kukisimamia na kukiendeleza Chuo cha Kilimo Kizimbani ili kiweze kutoa wahitimu bora na wenye sifa kwa lengo la kuendeleza kilimo nchini. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Chuo hicho kwa kushirikiana na Idara ya Umwagiliaji Maji na Mradi wa TANRICE unaofadhiliwa na JICA kimeweza kutoa mafunzo kwa wakulima 296 wa mpunga wa umwagiliaji maji katika mabonde ya Mtwango, Weni na Mangwena. Takwimu zinaonesha kuwa wakulima hawa wameweza kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 4 hadi 6 kwa hekta. Mafanikio haya yamepatikana kutokana na wakulima kukubali kutumia mbinu bora za kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji.Aidha, Chuo cha Kilimo Cha Kizimbani, kimeweza kupata usajili wa chuo katika Baraza la Vyuo vya Ufundi Tanzania (NACTE) na kimeanza kutumia mitaala inayotilia mkazo mahitaji ya soko la ajira. Kadhalika, Chuo kimeweza kutoa wahitimu vijana 69 (wanawake 43 na wanaume 26) waliomaliza mafunzo ya ngazi ya cheti (Certificate in General Agriculture) ambao wataajiriwa kwenye kazi za kilimo na huduma za ugani.Ndugu Wananchi,Itakumbukwa kuwa katika hotuba yangu ya uzinduzi wa Baraza la Wawakilishi la Nane mwezi Novemba 2010, niliahidi kuwa Serikali yetu itakamilisha barabara zilizoanza kujengwa na Awamu ya Sita, kujenga barabara mpya kubwa, kujenga barabara ndogo ndogo na kuzitunza ipasavyo. Utekelezaji wa ahadi hizo umefanyika na katika kipindi cha mwaka mmoja, miradi kadhaa ya ujenzi wa barabara umekamilika katika visiwa vya Unguja na Pemba. Mradi wa barabara za Vijijini Pemba, ambao ulizihusisha barabara za Mtambile-Kengeja-Mwambe, Mtambile-Kangani, Mizingani-Wambaa, Chanjamjawiri-Tundauwa, Kenya-Chambani na Chanjaani-Pujini umekamilika na barabara hizo nilizizindua tarehe 8 na 9 Januari, 2012 katika shamra shamra za sherehe za Mapinduzi. Ujenzi huu kwa jumla ni wa kilomita 44.5 ambao ulitekelezwa kwa msaada wa Serikali ya Norway na Serikali yetu ilichangia.Kadhalika, ujenzi wa barabara za Mkoa wa Kaskazini Pemba ambazo ni Wete-Gando na Wete-Konde bado unaendelea vizuri. Vile vile, matayarisho ya ujenzi wa barabara ya Mzambaraukarim-Mapofu, Chwale-Kojani, Kipangani-Kangagani, Mzambarautakao-Pandani-Finya na Bahanasa-Daya-Makongoni-Mtambwe unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia “Millenium Challenge Account” tayari yameanza.Ndugu Wananchi,Kwa upande wa Unguja, ujenzi wa barabara ya Amani-Dunga tayari umekamilika na barabara hiyo niliizindua rasmi tarehe 7 Januari, 2012 katika Sherehe hizi za Mapinduzi. Aidha, ujenzi wa barabara ya Mfenesini-Bumbwini unaendelea na upo katika hatua nzuri. Kuhusu matayarisho ya ujenzi wa barabara ya Jendele-Cheju-Kaebona, Kizimbani-Kiboje na Koani-Jumbi, ambazo zinaunganisha maeneo ya kilimo, umefikia hatua za mwisho za kumtafuta Mkandarasi.Matengenezo ya barabara mbalimbali za Mjini na Vijijini yanaendelea kufanyika kwa kiwango cha lami, kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara. Kwa upande wa Unguja barabara ya Mwanakwerekwe-Nyumbambili, Kwamchina-Nyumbambili na Mombasa-Mbuyumnene, zimefanyiwa matengenezo makubwa, pamoja na kuifanyia matengenezo mzunguko wa barabara (Round about) ya Magomeni. Kwa Pemba, barabara inayotokea Weni hadi mzunguko wa barabara (Round about) ya Ikulu Wete inaendelea kufanyiwa matengenezo makubwa kwa kiwango cha lami.Kwa mara nyengine tena, nawatahadharisha madereva wa vyombo vya moto wazingatie na wazifate sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepuka ajali zisizo za lazima na baadhi ya wakati zinaweza kusababisha vifo, ulemavu na uharibifu wa mali. Serikali inaendelea na juhudi mbali mbali za kudhibiti ajali za barabarani. Nasaha zangu kwenu ndugu wananchi, ni kutumia barabara kwa uangalifu, kufuata sheria za usalama barabarani na kushirikiana kikamilfu na taasisi zinazohusika na suala hili. Ubora wa barabara zetu uwe ni faraja na katu usituletee majonzi.Ndugu Wananchi,Katika kuimarisha huduma za usafiri wa anga, Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar wa Abeid Amani Karume. Ujenzi huo unafanywa na Kampuni ya Kichina Beijing Engineering Construction kwa mkopo wa US$ 70.4 milioni kutoka Exim Bank ya China. Aidha, mwezi wa Disemba, 2011, Serikali imekamilisha taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa njia za kupitia ndege (Taxiway) na maegesho ya ndege (Apron), mradi ambao utatekelezwa kwa mkopo wa US$ 54 milioni kutoka Benki ya Dunia.Ndugu Wananchi,Kwa upande wa usafiri wa baharini Serikali inaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ujenzi wa gati mpya ya Mpigaduri. Tayari utafiti wa awali umeshafanywa na Serikali imefanya uchambuzi wa taarifa za utafiti huo. Aidha, Serikali inaendelea na juhudi zake za kutafuta usafiri wa uhakika na wa kisasa utakaowawezesha abiria na mizigo yao kusafiri baina ya kisiwa cha Unguja na Pemba, kwa usalama na bila ya usumbufu. Tunawashukuru wafanyabiashara ambao tayari wameanza kutoa huduma za usafiri wa baharini katika kisiwa cha Unguja na Pemba. Jitihada zao hizo tunazithamini sana.Ndugu Wananchi,Katika kuimarisha huduma za mawasiliano Serikali inaendelea na hatua za kusimamia taasisi zote zinazotoa huduma za mawasiliano ya simu kwa kupunguza ongezeko kubwa la ujenzi wa minara ya mawasiliano kwa Unguja na Pemba. Aidha, Serikali inasimamia mradi mkubwa wa mawasiliano wa “e-government” ambao utarahisisha mawasiliano ya taasisi zote za Serikali za Unguja na Pemba na matumizi mengine mbali mbali.Mradi huo unatekelezwa kwa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 20 kutoka Benki ya Exim ya China. Katika utekelezaji wa mradi huu hivi sasa Serikali imeshatayarisha jengo hapo Mazizini ambalo litakuwa ni kituo cha mtandao huo na kazi nyengine zote zinaendelea vizuri.Ndugu Wananchi,Suala la kutoka katika mfumo wa analojia na kuingia kwenye mfumo wa digitali ifikapo tarehe 31 Disemba, 2012 ni la lazima kwa nchi zote na kwa msingi huu nasi Zanzibar tunahusika.Serikali imeshajiandaa katika kukabiliana na mabadiliko hayo kwa kuchukua hatua mbali mbali ikiwa ni pamoja na kufanya uchambuzi wa gharama, bei za vifaa vitakavyohitajika. Vilevile, Serikali imeziagiza taasisi zinazohusika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya teknolojia mpya na umuhimu wake. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba, tunaingia katika digitali kwa wakati uliopangwa bila ya kutokea athari yoyote.Ndugu Wananchi,Sekta ya Biashara ni miongoni mwa sekta muhimu katika maendeleo ya ukuzaji uchumi hasa ikizingatiwa nchi yetu ni kisiwa chenye eneo dogo kwa kuendeleza kilimo na mambo mengine yanayohitaji ardhi kubwa. Kwa kuzingatia umuhimu wa sekta hii, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za marekebisho ili kuimarisha mazingira ya ufanyaji wa biashara na kuweka usimamizi endelevu. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kuandikwa kwa Kanuni mpya za usimamizi wa biashara ambazo, pia, zitasimamia uagiziaji wa bidhaa mbali mbali zikiwemo, mchele, sukari na unga wa ngano. Kanuni hizi zimetayarishwa na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko na kuwashirikisha wafanyabiashara. Aidha, kwa lengo la kujenga ushindani katika soko la bidhaa za chakula, serikali inaendelea kuwakaribisha wenye uwezo kuingiza bidhaa nchini.Suala la ubora wa bidhaa zinazoingia nchini ni muhimu. Katika kulifanikisha lengo hili la Serikali, hivi karibuni Serikali imetunga Sheria ya Viwango Namba 1 ya mwaka 2011, ambayo itaanzisha Taasisi ya Viwango ya Zanzibar kwa ajili ya kusimamia ubora wa bidhaa.Ndugu Wananchi,Katika kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010/2015 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa imeendelea kuimarisha Mapinduzi ya Kilimo kwa kuendeleza uzalishaji wa mazao ya biashara hasa karafuu, matunda na viungo. Kuhusu zao la karaafuu umuhimu mkubwa umewekwa katika kuliimarisha, kuliendeleza na kutolibinafsisha na tarehe 28 Februari, 2011, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifikia uamuzi huo. Sambamba na uamuzi huo tarehe 11 Agosti, 2011 Serikali iliamua kuubadilisha muundo wa Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC) pamoja na kuyabadilisha majukumu yake; uamuzi huu ulipelekea kutungwa sheria mpya ya ZSTC.Katika kusimamia utekelezaji wa kuliimarisha na kuliendeleza zao la karafuu tarehe 2 Juni, 2011 niliyatembelea baadhi ya mashamba ya Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba na nilivutiwa sana na jitihada za wakulima wa karafuu hasa kule Junguni, Gando na Chanjaani Mwanamitaji, Chake Chake, kwenye kitalu cha mikarafuu.Kutokana na azma ya Serikali ya kuliimarisha na kuliendeleza zao la karafuu, tarehe 4 Juni, 2011, nilipokuwa nafanya majumuisho ya ziara yangu ya Mkoa wa Kusini Pemba, niliwaahidi wakulima wa karafuu kwamba Serikali itaweka bei nzuri yenye tija kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2011. Tarehe 3 Julai, 2011 Serikali ilitangaza bei mpya ya karafuu. Vile vile, niliahidi kwamba Serikali itatoa miche ya mikarafuu 500,000 kwa wakulima wa karafuu bure, kwa kila mwaka, kuanzia mwaka 2011; kwa kipindi cha miaka kumi (10) ijayo. Hadi hivi sasa Serikali tayari ishawapa wakulima wa Unguja na Pemba jumla ya miche 239,600.Katika bei iliyotangazwa tarehe 3 Julai, 2011, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuwalipa wakulima T.Shs. 10,000 kwa kilo moja ya karafuu badala ya T.Shs. 5,000 ya mwaka 2010. Bei hio iliongezwa hadi sasa kufikia TShs. 15,000 kwa kilo sawa na ongezeko la asilimia 300 kutokana na bei ya 2010 ya T.Shs. 5,000 kwa kilo. Hivi sasa mkulima analipwa asilimia 80 ya bei ya karafuu duniani.Kwa mara nyengine tena natoa shukurani kwa wakulima wote wa karafuu kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuliendeleza zao hili. Nimefarijika sana na hatua yao ya kuitikia wito wa Serikali wa kuziuza karafuu zote katika vituo vya Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC). Takwimu nilizonazo ni kwamba, hadi tarehe 10 Januari, 2012 jumla ya tani 4213.768 zimenunuliwa kwa TShs. 62,971,983,250.00. Ununuzi huo umepindukia makadirio ya kununua tani 3,000 kwa gharama ya T.Shs. 37.00 bilioni yaliyokisiwa kabla ya uchumaji na uuzaji wa karafuu haujaanza.Katika jitihada za kuliimarisha zao la karafuu, Serikali imeanzisha mfuko maalum wa kuendeleza zao hilo wenye lengo la kusaidia uzalishaji wa miche, na usambazaji wake, utafiti na utoaji wa elimu kwa wakulima. Pia, Serikali inaandaa mikakati ya kuzitafutia karafuu za Zanzibar hati miliki (Brand) kwa lengo ya kupata bei nzuri katika soko la dunia.Wito wangu kwenu wananchi nyote ni tuendelee kushirikiana katika kuliimarisha zaidi zao la karafuu na kupambana na magendo kwa kila hali, kama tulivyofanya mwaka huu. Natoa shukurani kwenu wananchi, Kikosi Kazi Maalum cha Karafuu, Idara Maalumu za SMZ na Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kwa mafanikio haya. Serikali itaendelea kuwapa wakulima bei nzuri, kila bei ya karafuu itakapopanda kwenye soko la dunia na kuwalipa pesa zao taslim bila ya kuwakopa na bila ya kuchelewa.Ndugu Wananchi,Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na viwanda ili kuongeza vyanzo vya mapato, kurahisisha upatikanaji wa bidhaa mbali mbali na kutoa fursa zaidi za ajira kwa wananchi wetu. Serikali imekamilisha utafiti na kutathmini uwezekano wa kuifanya Zanzibar kuwa eneo tengefu (SEZ) la kiuchumi na sasa Serikali inauzingatia utafiti huo kwa ajili ya kuandaa mpango wa utekelezaji wake.Ndugu Wananchi,Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Serikali imefanya juhudi maalum za kuuimarisha utumishi wa umma na utawala bora. Katika kutekeleza na kuimarisha utawala bora, Serikali imetayarisha Sera ya Utawala Bora, iliyopelekea kutayarishwa kwa Msaada wa Sheria ya Kuzuia Rushwa, ambao unatarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi cha Januari, 2012. Vile vile Serikali inaendelea na hatua ya kuandaa sheria ya Maadili ya Viongozi ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika. Aidha, Serikali imetayarisha Rasimu ya Awali ya Sera ya Mawasiliano ya Elektroniki yenye lengo la kuweka mfumo wa kisasa wa utoaji wa huduma za umma. Kadhalika rasimu ya Sera ya Usafiri (kwa watumishi wa Serikali) nayo imetayarishwa. Sera hii ina lengo la kuweka mfumo bora wa usafiri utakaohakikisha kuwepo kwa utaratibu na muongozo wa upatikanaji wa huduma za usafiri kwa watumishi wa umma. Hivi karibuni Rasimu ya Sera hio tayari imepelekwa kwa wahusika mbali mbali wa Unguja na Pemba ili waweze kutoa maoni yao.Kama nilivyoahidi mwaka jana kwamba Serikali itaandaa sheria mpya ya utumishi wa umma yenye lengo la kuleta ufanisi kazini, kuwatumikia wananchi bila ya upendeleo au bughudha na kuzitatua kero zao kwa wakati na huku wafanyakazi nao wakipata haki zao kutokana na kutimiza wajibu wao. Kama mjuavyo, sheria hio ilipitishwa na Baraza la Wawakilishi na baada ya kuiridhia hapo tarehe 1 Julai, 2011, hivi sasa tayari inatumika.Katika kuuimarisha utumishi wa umma, Serikali imeipitia upya miundo ya utumishi na kufanyiwa marekebisho, ili watumishi wawekwe katika daraja zao, waweze kuitambua mishahara yao na stahili nyengine wanazostahiki kupewa pamoja na kuufahamu utaratibu wa kupandishwa vyeo.Vile vile, katika kipindi hiki Serikali imepandisha mshahara na kuwalipa wafanyakazi viwango vipya, pamoja na kuwalipa viwango vipya vya posho mbali mbali wale wafanyakazi waliostahiki posho hizo. Maslahi hayo mapya ya wafanyakazi mbali mbali wa Serikali yalilipwa kuanzia mwezi wa Oktoba, 2011. Aidha, Serikali itaendelea kuyafanyia kazi malalamiko yote ya msingi kuhusu mishahara mipya yanayofikishwa kwenye Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora.Pamoja na kuipandisha mishahara na posho na kuendelea kulipa mishahara ya wafanyakazi wote wa Serikali kwa wakati, Serikali hadi kufikia mwezi wa Novemba, 2011 imelipa mafao ya kiinua mgongo kwa wastaafu wote. Kutokana na juhudi zetu za kukusanya mapato kwa mafanikio yenye kutia moyo, Serikali itaendelea kuyaimarisha maslahi ya wafanyakazi, kila uwezo wetu unapoimarika; kwani Waswahili wamesema “Mcheza kwao hutunzwa”. Hata hivyo, ninatarajia kwamba wafanyakazi nao kwa upande wao wataendelea kutimiza wajibu wao, kutoa huduma nzuri na zitakazotolewa kwa misingi ya uadilifu na inayozingatia sheria.Ndugu Wananchi,Miongoni mwa malengo ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ni kuwapatia makaazi bora na ya kisasa wananchi wenye kipato cha chini, kwa hivyo, katika mwaka uliopita Serikali inaendelea na hatua za ujenzi wa nyumba bora za maendeleo huko Mpapa, ujenzi huo upo katika hatua nzuri za kumalizika. Serikali itaendelea na juhudi za ujenzi wa nyumba bora za maendeleo katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu. Kadhalika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya uamuzi wa kuzifanyia matengenezo nyumba za maendeleo za Serikali na kazi itaanza kwa nyumba zilioko Kengeja huko Pemba.Kwa upande wa wazee wetu wanaoishi Sebleni na Gombani, Serikali itaendelea kuwatunza wazee hao na kuwasaidia ili waweze kuyakimu maisha yao. Jitihada tulizozichukua za kuzifanyia matengenezo nyumba wanazoishi zitaendelezwa. Posho kwa ajili ya matumizi tayari zimeongezwa na zitaendelezwa kuongezwa. Kadhalika, watoto wetu tutaendelea kuwapa elimu ya lazima, tutawatunza dhidi ya udhalilishaji wa aina yoyote ile na tutawalinda kwa kuzingatia sheria ya mtoto ya mwaka 2011.Ndugu Wananchi,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuutekeleza mradi wa Maendeleo ya Miji (Zanzibar Urban Services Project –ZUSP) kama ilivyofikia makubaliano na Benki ya Dunia yalioanza tarehe 6 Aprili, 2011, kutiwa saini mkataba mwezi wa Mei, 2011 na kuanza rasmi tarehe 11 Julai, 2011. Mradi huo utaimarisha haiba ya miji, mazingira ya usafi na kuwa kivutio cha watalii ndani ya Manispaa ya Zanzibar na Miji ya Chake Chake, Mkoani na Wete Pemba. Mradi huo utaimarisha michirizi ya maji ya mvua katika maeneo mbali mbali pamoja na eneo la Mnazi mmoja, udhibiti wa taka, uwekaji wa taa za barabarani katika Mji Mkongwe, mipango ya ardhi na makaazi na kuyaimarisha Mabaraza ya miji yanayohusika katika kusimamia na kuendeleza huduma mbali mbali kwa ufanisi. Jumla ya T.Shs. 57 bilioni zitatumika katika mradi huo.Hadi kufikia tarehe 10 Disemba, 2011; utoaji wa Zabuni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kazi mbali mbali, imekamilika.Ndugu Wananchi,Maji ni uhai, hii ni kauli mbiu inayotumika ulimwengu mzima. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuithamini kauli mbiu hio imekuwa ikifanya juhudi mbali mbali za muda mrefu katika kuwapatia wananchi maji safi na salama nchini.Baada ya kukamilika awamu mbili za mradi wa Japan kupitia Shirika la JICA, jitihada za upatikanaji maji kwenye Mkoa wa Mjini Magharibi zinaendelezwa na Serikali. Hivi sasa uchimbaji wa visima tisa (9) kwa ajili ya Mkoa wa Mjini unaendelea. Kadhalika, kwa kupitia Serikali ya Watu wa China mpango wa kuchimba visima 23, ulazaji wa mabomba na ujenzi wa matangi utaanza hivi karibuni Unguja na Pemba. Kadhalika, Serikali imechukua mkopo wa T.Shs. 33 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika katika kugharamia upatikanaji wa maji. Fedha hizi zitatumika kwenye mradi wa Uimarishaji Miundombinu ya maji, ikiwemo ujenzi wa visima.Aidha, mkopo uliotolewa na ADB wa T.Shs. 67 bilioni, kufuatia mkataba uliotiwa saini tarehe 22 Disemba, 2008 kwa ajili ya uimarishaji wa huduma za maji katika miji mitatu ya Pemba na baadhi ya maeneo ya vijiji vya Unguja na Pemba utatumika kwa uchimbaji wa visima, ulazaji wa mabomba, ujenzi wa matangi pamoja na kuiongezea uwezo Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA); kazi ambayo imekwishaanza tangu Septemba, 2011.Nataka nitumie nafasi hii niipongeze Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati pamoja na ZAWA kwa jitihada walizozichukua kuwapelekea maji wakazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi na maeneo mengine katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Walifanya jitihada hizo kwa kuwapelekea wananchi maji kwa kutumia magari makubwa pale ambapo maji yalikuwa hayapatikani.Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa kununua vifaa ili kuimarisha miundombinu, kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuvihifadhi vianzio vya maji, kwa kupanda miti na kutojenga nyumba za kuishi katika maeneo hayo.Ndugu Wananchi,Serikali imeendeleza kazi ya kusambaza umeme katika maeneo mbali mbali kwa ujenzi wa njia kubwa na ndogo za umeme katika vijiji mbali mbali vya Unguja na Pemba. Juhudi za makusudi zinafanywa na Serikali ili kuhakikisha kwamba huduma za umeme wa uhakika unapatikana Zanzibar. Serikali inaendeleza mradi wa umeme kwa kulaza waya mpya wa umeme unaopitishwa chini ya bahari kutoka Tanzania Bara wenye thamani ya US$ 72.0 milioni unaogharamiwa na Shirika la “Millennium Challenge Corporation” la Marekani zikiwemo US$ 1.5 zitakazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Utengenezaji wa waya wa kupitisha umeme kutoka Tanzania Bara hadi Ras Fumba, Zanzibar, imeshakamilika kwa asilimia 90 na mnamo mwezi wa Julai mwaka huu waya huo unatarajiwa kuletwa Zanzibar. Kazi ya kutengeneza waya huo inafanywa na Kampuni ya VISCAS CORPORATION ya Japan. Kazi nyengine za mradi huu zinaendelea vizuri kama zilivyopangwa. Mradi huu utakapomalizika utaondoa kero ya umeme wa mgao kwa wananchi na wafanyabiashara wote kwa jumla.Ndugu Wananchi,Mnamo mwezi wa Machi 2011 Serikali ilitia saini mkataba wa US$. 35 milioni na Serikali ya Japan wa kusaidia ujenzi wa vituo na njia za kusambazia umeme Unguja na Pemba. Lengo la Serikali kwenye mradi huo ni kuwapa wananchi huduma bora za umeme kwenye maeneo yote ya mjini na mashamba.Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kupitia Shirika lake la Umeme ZECO, limefanikiwa kuwaungia huduma za umeme wateja wapya 3,529 Unguja na Pemba. Jambo la kufurahisha ni kuwa wateja wengi walioungiwa umeme wanatoka vijijini. Hatua hii imefikiwa baada ya Shirika la Umeme kuruhusiwa kuwaungia umeme wananchi wenye kipato cha chini, kwa njia ya mkopo.Ndugu Wananchi,Katika kutimiza malengo ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010/2015, MKUZA II na Sera ya Afya. Huduma za kinga na tiba zimeendelea kutolewa kwa ufanisi, katika hospitali zote na kwenye vituo vya afya.Mpango Mkakati wa kuifanya Hospitali ya Mnazimmoja ifikie hadhi ya Hospitali ya Rufaa tayari umeandaliwa kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani. Vile vile, utaratibu wa mahitaji ya kulifanyia ukarabati jengo kubwa la Hospitali ya Mnazimmoja unaendelea kutayarishwa kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kiarabu, BADEA. Kadhalika, Mpango wa kukibadilisha kiwanda cha dawa kiliopo katika eneo la Hospitali ya Mnazimmoja ili kitumike kwa ajili ya matumizi ya vitengo mbali mbali vya Hospitali ya Mnazimmoja hivi sasa unaandaliwa kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi na hivi karibuni matengenezo yataanza.Huduma za uchunguzi wa maradhi zimeimarishwa pamoja na kufanyiwa matengenezo jengo la maabara ya uchunguzi wa maradhi (Pathology laboratory); na pia zana za kisasa kwa ajili ya uchunguzi wa maradhi tayari zimepatikana kwa msaada wa Shirika la Kimarekani la “International Centre for Aids Care and Treatment Programs”. Jitihada hizi zitasaidia sana katika kuyachunguza maradhi kwa wakati ili tiba sahihi iweze kutolewa. Mipango mengine imeandaliwa ya kuhakikisha mafunzo ya madaktari yanayotolewa na madaktari wa Cuba yanaendelezwa. Kadhalika, masomo ya “Biomedical Engineering” yataanza kutolewa katika Chuo cha Sayansi za Afya, Mbweni.Kuhusu kuipandisha hadhi Hospitali ya Abdulla Mzee ya Mkoani kuwa Hospitali ya Mkoa, Serikali ya Watu wa China imekubali kuifanyia matengenezo makubwa hospitali hii ili iweze kutoa huduma bora zaidi. Wataalamu kutoka China walifika Zanzibar mwezi wa Oktoba kwa mazungumzo ya awali.Vile vile, Serikali tayari imeanza kuchukua hatua za kuipandisha daraja Hospitali ya Cottage ya Makunduchi na kuwa hospitali ya wilaya kwa kushirikiana na shirika lisilokuwa la kiserikali la Uingereza liitwalo “Health Improvement Project”. Huduma za afya katika hospitali hii, sasa zimeimarika. Kuanzia mwaka huu, huduma za aina hii zitaimarishwa katika Hospitali ya Cottage ya Kivunge ili nayo baadae ifikie kiwango kilichofikiwa na Hospitali ya Makunduchi.Ndugu Wananchi,Huduma nyengine za afya, kama vile mapambano dhidi ya malaria zinaendelea vizuri huku tukilenga kuyaondoa kabisa maradhi haya hapa Zanzibar, ambapo kwa sasa malaria imefikia kiwango cha asilimia 0.6.Aidha, vifo vya watoto wachanga vimepungua na vimefikia idadi ya 51/1,000 mwaka 2011, badala ya 57/1,000 ya makisio ya 2010, vile vya watoto walio chini ya miaka mitano vimefikia 73/1,000 ikilinganishwa na makisio ya MKUZA 71/1,000 ya 2010. Hata hivyo, lengo la kuvipunguza vifo vya akinamama vinavyotokana na uzazi lililowekwa na MKUZA la 251/100,000 hapo 2010, bado halijafikiwa. Kwa mwaka 2011 idadi ya vifo hivyo ni 287/100,000. Serikali itafanya kila jitihada, ili lengo la MKUZA liweze kufikiwa.Kuhusu UKIMWI, hadi kufikia Septemba, 2011, jitihada za kupambana nao zimeendelea kwa kasi nzuri. Huduma za upimaji wa virusi vya UKIMWI kwa hiari imeendelea kutolewa katika vituo 56 Unguja na Pemba. Wagonjwa 5676 wamesajiliwa na kupatiwa huduma katika vituo 10 vya kupunguza makali Unguja na Pemba. Kati ya wagonjwa hao, wagonjwa 313 wanapewa dawa za kupunguza makali (ARVs).Katika kupambana na maradhi yasiyo ya kuambukiza hasa maradhi ya saratani, maradhi ya moyo na matatizo ya figo, Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukland cha Norway, tarehe 5 Septemba 2011, ililikubali ombi la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kutoa msaada wa kuanzishwa vitengo hivyo na bingwa wa maradhi hayo amefika nchini tarehe 8 mwezi huu kwa kuandaa mpango wa utekelezaji kwa mujibu wa mahitaji ya Wizara ya Afya.Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Serikali imeanza kujenga ghala la dawa la kisasa huko Maruhubi litakalogharimu US$ 1.2 milioni kwa msaada wa Serikali ya Marekani na Denmark kupitia Shirika la USAID na DANIDA.Ndugu Wananchi,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imeendelea kutoa kipaumbele katika suala la kuwapatia vijana wetu elimu iliyo bora katika ngazi zote za elimu. Serikali imefanikiwa kuongeza idadi ya skuli zinazotoa elimu ya maandalizi kutoka skuli 238 mwaka 2010 na kufikia 244 mwaka 2011. Katika kipindi hiki, skuli za msingi zimeongezeka kutoka 148 mwaka 2010 hadi 156 mwaka 2011. Idadi ya madarasa mapya 120 nayo imeongezeka katika kipindi hiki cha mwaka mmoja.Aidha, kutokana na kuongezeka kwa ujenzi wa skuli na madarasa mapya, uandikishaji wa watoto wenye umri wa kuanza darasa la kwanza umeongezeka kutoka wanafunzi 38,743 mwaka 2010 hadi 41,293 mwaka 2011 ambapo kila mtoto aliyefikia umri wa kwenda skuli, amepatiwa fursa hiyo. Idadi ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba na kujiunga na kidatu cha kwanza imeongezeka kutoka 25,973 mwaka 2010 hadi 26928 mwaka 2011.Pia, skuli za sekondari zenye kidato cha I hadi cha V1 zimeongezeka kutoka 99 mwaka 2010 hadi 103 mwaka 2011. Pia, ujenzi wa skuli mpya za kisasa 21 za Wilaya za Unguja na Pemba nilizoziahidi kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010/2015 tayari skuli 16 kati ya hizo zitakamilika hivi karibuni. Kukamilika kwa skuli hizo 16 (8 zipo Unguja na 8 zipo Pemba) kutatoa fursa kwa vijana wengi zaidi kupata elimu ya sekondari katika skuli zenye mazingira bora na vifaa vya kisasa. Serikali itafanya kila jitihada ili kila mwanafunzi anayefaulu kuingia skuli ya sekondari asikose kusoma. Aidha, matayarisho ya ujenzi wa skuli nyengine za sekondari tano zilizobakia nazo ujenzi wake utaanza hivi karibuni.Serikali imeendelea kushughulikia fursa za upatikanaji wa elimu ya juu kwa kiwango cha shahada ya kwanza kwa vijana wake. Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA kinaendelea kuimarishwa ili kiweze kutoa taaluma bora, ushauri na kufanya tafiti zitazosaidia kukabiliana na changamoto za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.Aidha, katika mwaka 2010/2011 jumla ya wanafunzi 324 walihitimu mafunzo yao na kutunukiwa shahada mbali mbali, ambapo 14 walitunukiwa vyetu, 210 stashahada na 100 shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Taifa (SUZA) katika mwaka wa masomo 2010/2011.Kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi wa Zanzibar, Serikali kupitia Bodi ya Mkopo wa Elimu ya Juu imeweza kuwagharamia jumla ya wanafunzi wapya 209 kwa mwaka 2011/2012, kati ya wanafunzi 1,800 waliopeleka maombi ya mikopo. Ili kuwahudumia wanafunzi wote 1,800 walioomba mikopo, jumla ya T.Shs. 15.3 bilioni zilihitajika. Fedha zilizoidhinishwa na Serikali kwa mwaka huu wa fedha ni T.Shs. 4.0 bilioni ambapo jumla ya T.Shs. 1.5 bilioni ndio zilizokabidhiwa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu hadi sasa.Kwa hakika kiwango cha fedha kilichoidhinishwa na kutolewa ni kidogo kulingana na idadi ya wanafunzi wanaohitaji kupatiwa mikopo ya elimu ya juu. Hii ni changamoto kubwa inayoikabili Serikali kwa hivi sasa katika sekta ya elimu. Ninatarajia kuwa wanafunzi na wazazi wataifahamu changamoto tuliyonayo na uchache wa fedha za mikopo. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itaendelea na juhudi za kuimarisha mfuko huu, ili uweze kuwasaidia wanafunzi wengi zaidi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.Ndugu Wananchi,Mafanikio ya huduma za jamii yanategemea sana kwa kupatiwa habari na taarifa sahihi. Serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya habari kuwa ni huduma muhimu. Katika kuimarisha sekta ya habari, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, imeunda Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) kama nilivyoahidi mwaka jana katika maadhimisho ya miaka 47 ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kuiunganisha Televisheni ya Zanzibar (TVZ) na Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ). Katika kuimarisha televisheni na redio, Serikali kupitia shirika hili imeshakamilisha ufungaji wa transmita mpya za kurushia matangazo ya Televisheni kwa Pemba na Unguja. Kukamilika kwa kazi hiyo, kutaimarisha hali ya utazamaji wa vipindi vya televisheni ya Shirika la Utangazaji Zanzibar, kwa Zanzibar yote na hasa Pemba, ambako kwa kipindi kirefu huduma za Televisheni zilikosekana.Kwa mafanikio makubwa Serikali imeweza kuuhamisha mnara wa matangazo ya Redio ya Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) wa masafa ya kati uliokuwepo Chumbuni na kuupeleka katika eneo la Bungi. Uamuzi huu umefikiwa kwa sababu mnara huo ulikuwepo katika sehemu ya njia ya kuanzia kutulia ndege zinazoingia Zanzibar. Tatizo hili lilisababishwa na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.Kwa upande wa matangazo ya redio, Serikali imeendelea kuimarisha huduma za matangazo na hivi sasa wataalamu kutoka Jamhuri ya Watu wa China wanaendelea kuifanyia matengenezo baadhi ya mitambo yake. Aidha, gazeti la Zanzibar Leo nalo limeimarika kwa ubora wake na sasa linahimili ushindani, umaarufu wake umezidi na idadi ya wateja wake imeongezeka. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya kila jitihada ili gazeti hili lichapishwe katika mitambo ya Serikali hapa Zanzibar.Kwa upande wa uimarishaji wa sekta ya Michezo, Serikali imeendelea kuwahamasisha Wazanzibari kuimarisha michezo ili kujenga afya zao na kuiletea sifa nchi yetu kwa kushiriki mashindano mbali mbali ya kimataifa. Miongoni mwa hatua tulizochukua mwaka 2011 ni kukamilisha utandikaji wa nyasi za bandia katika uwanja wa Gombani Pemba. Uwanja huo tayari umeanza kutumika kwa kuchezewa mechi za kitaifa. Kwa upande wa mchezo wa mpira wa miguu, timu yetu ya Zanzibar Heroes inafanya vizuri ingawa katika mashindano ya mwaka huu ya Afrika Mashariki na Kati hatukupata ushindi. Hata hviyo, nidhamu ya timu yetu na inavyojituma tunataraji kupata mafanikio hapo baadae. Michezo mengine, mpira wa wavu, wa pete na riadha tumeendelea kuonesha jitihada.Vile vile, Serikali inaendelea kukuza na kulinda utamaduni wa Mzanzibari ambao una historia ya pekee kwa kuunga mkono shughuli mbali mbali za utamaduni zikiwemo matamasha, michezo ya asili na maonesha ya sanaa ya asili ya Mzanzibari, filamu na muziki, likiwemo Tamasha la Mzanzibari, Tamasha la Sauti za Busara, Tamasha la Nchi za Jahazi (ZIFF) na “Jahazi Lateral and Jazz Festival” ambayo hufanyika hapa Zanzibar. Matamasha haya hutoa mafunzo, hukonga nyoyo za jamii pamoja na kukuza uhusiano miongoni mwa watu wa nchi mbali mbali.Kadhalika, tumeanza kutekeleza ahadi yetu ya kujenga studio mpya ya kurekodia kazi za wasanii wetu kwa lengo la kulinda na kuhifadhi kazi zao kwa faida yao na sote kwa jumla. Fedha za kuanzia kazi hio zimetengwa kwenye bajeti ya mwaka 2011/2012.Ndugu Wananchi,Utalii ni sekta kiongozi katika utekelezaji MKUZA II inayotegemewa sana kwa kukua uchumi wetu na kupunguza umaskini. Kwa makadirio ya mwaka 2010, jumla ya US$ 104.3 milioni zinatokana na sekta hii. Watalii wanaoingia nchini wamekuwa wakiongezeka na jumla ya watalii walioingia Zanzibar mwaka 2011 kutoka nchi za nje ni 175,063. Idadi hii ni kubwa ambayo haijawahi kurikodiwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Kabla ya mwaka 2011, idadi ya juu kabisa ya watalii ni mwaka 2007 ambapo jumla ya watalii 143,282 waliingia nchini. Ukuaji wa utalii ni asilimia 6 kwa mwaka na asilimia 72 ya wawekezaji wote wamewekeza kwenye sekta ya utalii.Mwezi wa Septemba, 2011 Serikali imeanzisha kaulimbiu ya “Utalii kwa Wote” katika kuitekeleza MKUZA II ambapo utalii ni sekta kiongozi. Lengo la kaulimbiu hii ni kuwashirikisha wananchi wa Zanzibar kuiunga mkono Serikali yao kwenye suala hili muhimu la maendeleo. Mipango madhubuti inaandaliwa katika kulitekeleza suala hili.Napenda kutoa wito kwa Kamisheni ya Utalii na wahusika wengine wa Sekta hii kuendeleza na kuimarisha utalii wa kumbukumbu za kihistoria, utalii wa kiutamaduni na utalii wa ndani wenye kutunza mazingira. Aidha, kuibua maeneo mapya ya vivutio vya utalii yakiwemo mapango, magofu, maeneo ya historia, michezo ya asili na matamasha kwa lengo la kuongeza idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini mwetu.Ndugu Wananchi,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuwapatia ajira wananchi wake ili kupunguza umasikini. Katika mwaka 2011, Serikali imehamasisha na kusajili vyama vya ushirika 212, Unguja na Pemba na kuifanya idadi yake kuwa 5,936. Mafunzo yalitolewa kwa wanachama 11,417 wa vyama 434. Aidha vikundi 52 vya ufugaji nyuki vimepatiwa mafunzo na kituo cha kisasa cha usafishaji asali kimejengwa hapa Kitogani. Uzalishaji wa asali umeongezeka kutoka Tani 1.5 mpaka Tani 5 na kuwapatia wafugaji wa nyuki T.Shs. 42.2 milioni.Aidha, jumla ya wananchi 190 walipatiwa mikopo ya T.Shs. 108.60 milioni kupitia Mfuko wa Kujitegemea katika mwaka 2011. Pia, T.Shs. 44.00 milioni zimetumika kwa wakopaji 11 kutoka mfuko wa AK na JK mwaka 2011. Kadhalika, Serikali ya Norway, kupitia UN HABITAT, katika mwaka 2011, uliipatia Zanzibar T.Shs. 149.00 milioni ambapo T.Shs. 13.00 milioni zilitumika kwa mafunzo ya vikundi. Pia, T.Shs. 136.00 milioni wamepatiwa vikundi sita vilivyofanikiwa kwa mwaka 2011.Ndugu Wananchi,Zanzibar ni kisiwa na bahari inawafanya wananchi wake wengi kuitegemea kama ni chanzo kikuu cha kujipatia kipato. Serikali inaendelea kufanya jitihada za kuwapa taaluma wavuvi ili waendeleze uvuvi uwe wenye tija. Katika kufikia lengo hilo, vikundi 85 vya wanavijiji vimeshajiishwa kuhusu ufugaji bora wa samaki, kaa, na chaza ili waweze kuongeza kipato chao. Kadhalika, hivi karibuni wazalishaji wa mazao ya baharini 30 wakiwemo wajasiriamali 18 na wataalamu 12 walipelekwa China kwa mafunzo ya ufugaji wa samaki, kamba, chaza nakadhalika.Sekta ya uvuvi imeonesha mafanikio makubwa na kwa sasa mchango wake katika Pato la Taifa umefikia asilimia 6. Katika mwaka 2010/2011 jumla ya tani za samaki 26,600 zilivuliwa zenye thamani ya T.Shs. 61.00 bilioni. Haya ni mafanikio makubwa yanayopaswa kuendelezwa. Kwa upande wa mwani, katika mwaka 2010/2011 Zanzibar ilivuna tani 12,500. Kutokana na jitihada hizi za wakulima wa mwani, Serikali itawashajiisha wanunuzi wa mwani wafikirie kuongeza bei.Ndugu Wananchi,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na mchakato wake wa kusajili watu wenye ulemavu kupitia katika shehia zao, zaidi ya watu wenye ulemavu 9,000 wameshajiliwa wakiwemo 3007 Kaskazini Unguja, 6,434 kutoka Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba.Ili kuifanya Sera na Sheria iendane na wakati Serikali imeanza kufanya mapitio ya sera ya watu wenye ulemavu ya 2004, ili kujadili changamoto mbali mbali zinazoikabili sera hiyo kwa maslahi ya watu wenye ulemavu hapa Zanzibar.Aidha, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwa na maafisa waratibu katika taasisi zote za umma, ili kujumuisha masuala ya watu wenye ulemavu na kupatikana kwa mahitaji yao, kuzifanya shughuli zao zitekelezeke kiurahisi katika taasisi zote za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kutekeleza mkataba wa Kimataifa wa Haki na Fursa za watu wenye ulemavu.Ndugu Wananchi,Zanzibar imekabiliwa na changamoto nyingi za kimazingira ikiwa ni pamoja na ukataji wa miti ovyo, utupaji ovyo wa taka, maji machafu yanayotiririka katika maeneo mengi, uchimbaji wa mchanga, mawe na kadhalika; bidhaa chakavu kadhaa zilizoingizwa za umeme, elektroniki na mifuko ya plastiki.Aidha, suala la mabadiliko ya tabianchi limekuwa ni tishio katika sehemu mbali mbali za dunia pamoja na Zanzibar. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea na jitihada kubwa za kuendelea kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuyatunza mazingira.Katika suala hili la uhifadhi wa mazingira, Serikali inathamini sana kuwepo kwa misitu ya asili na miti ya matunda. Misitu ya asili na miti ya matunda ni muhimu kwa kuhifadhi mazingira na kuchangia uchumi wetu. Katika kipindi cha mwaka uliopita jumla ya miche 1,280,300 ya aina mbali mbali imetolewa kwa ajili ya kupandwa na wananchi ili kurejesha rutba ya ardhi. Aidha, miche 25,000 imepandwa katika maeneo yalioathirika na uchimbaji wa mchanga na wastani wa hekta 20 tayari zimeimarishwa na gesi ya kupikia yenye thamani ya T.Shs. 125.2 milioni imetolewa kwa kaya 1,500 bila ya malipo kwa lengo la kutumia nishati mbadala ya kuni.Serikali imechukua hatua mbali mbali za kuzuwia uharibifu wa mazingira kutokana na utumiaji wa mifuko ya plasitiki. Miongoni wa hatua hizo ni kuundwa kwa kikosi maalum kinachosimamia utekelezaji wa sheria iliyoundwa inayokataza utumiaji wa mifuko hiyo, Pia, Serikali inaendelea kuwaelimisha wananchi juu ya madhara ya mifuko ya plastiki kwa mazingira yetu. Hatua hizo zimeshaanza kuzaa matunda mazuri.Ndugu Wananchi,Dawa za kulevya ni miongoni mwa changamoto zinazokabili nchi yetu na zinapoteza vijana kwa wingi kutoka na madhara yake. Ni lazima tuwanusuru vijana wetu. Serikali itaendelea na mapambano dhidi ya uingizaji na matumizi ya dawa hizi na tayari imekamilisha mswada wa marekebisho ya Sheria ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya.Ushiriki wa kila mtu katika vita hivi ni muhimu. Vile vile, mafunzo yanatolewa kwa vijana wanaoishi katika nyumba za walioacha kutumia dawa “Sober Houses”, ambazo hivi sasa zimefikia tisa (9). Matokeo yake ni kwamba vijana wanaotumia dawa za kulevya na kuranda ovyo huku wakisumbuwa wananchi wamepungua mitaani kwetu. Hali hii inatoa matumaini kwamba tukiendeleza ushirikiano tatizo hili tunaweza kulipunguza kwa asilimia kubwa na baadae tunaweza kulimaliza kabisa.Ndugu Wananchi,Wakati tunaposherehekea miaka 48 ya Mapinduzi ningependa kuwakumbusha wananchi kuwa Sensa ya Taifa ya Watu na Makaazi itafanyika mwaka huu. Hili ni tukio muhimu katika nchi yetu kwa sababu inapojulikana idadi ya watu ndipo upangaji bora wa huduma za uchumi na jamii unavyofanyika kwa ufanisi. Zoezi hilo litafanyika tarehe 26 Agosti, 2012.Tukio hili ni la kila baada ya miaka 10 kama ilivyopangwa na Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu. Sensa ya mwisho ilikuwa mwaka 2002 ambapo Zanzibar ilionekana kuwa na jumla ya watu 981,754, wakiwemo 620,957 Unguja na 360,797 Pemba. Sensa hiyo ilionesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la idadi ya watu ikilinganishwa na jumla ya watu 354,360 kufuatana na Sensa ya mwaka 1967. Bila ya shaka, kila mmoja wetu atapenda kujuwa tuko watu wangapi hivi sasa, miaka 48 baada ya Mapinduzi. Jawabu ya suala hili ni kwa kila mmoja wetu ashiriki katika zoezi hili.Natoa wito kwa watu wote tushirkiane kwenye suala hili na tuondoe hofu katika kujibu maswali tutakayoulizwa na maofisa watakaoifanya kazi hiyo.Ndugu Wananchi,Baada ya maelezo yangu juu ya tathmini ya mafanikio ya Zanzibar katika kipindi cha miaka 48 ya Mapinduzi sambamba na mafanikio tuliyoanza kuyapata katika mwaka wa kwanza wa awamu hii ya saba ya Serikali ya Mapinduzi yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa, sasa napenda nizungumzie kidogo juu ya mambo mengine ya msingi. Miongoni mwa mambo hayo ni uimarishaji wa Muungano wetu. Serikali zote mbili na wananchi wake tunaendelea kushirikiana vyema wakati tumo mbioni kuzipatia ufumbuzi wa kero mbali mbali zilizojitokeza ndani ya kipindi chote cha Muungano wetu tangu ulipoanzishwa tarehe 26 Aprili, 1964. Baadhi ya kero hizo ambazo mara nyingi tumekuwa tukizieleza zimeshapatiwa ufumbuzi na Kamati maalumu inayoongozwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Vile vile, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa pamoja zilishirikiana kikamilifu katika matayarisho ya Mswada wa Sheria wa kuweka utaratibu wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Katika mchakato wa kuandaa Katiba mpya, natoa wito kwenu wananchi mjitokeze kwa wingi kutoa maoni yenu bila ya hofu wala wasiwasi. Toeni maoni yenu mkiwa huru. Msiwe na woga na wala msitoe maoni hayo kwa njia ya jazba. Katiba inayokusudiwa kutungwa ni ya wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa hivyo, Wazanzibari ni haki yenu. Hakuna atakayewabeza. Napenda niwaase wale wote wenye tabia ya kuyadharau maoni ya wenzao, huu si wakati wa kufanya hivyo. Huu ni wakati wa kila mmoja kutoa maoni yake anavyoamini kwamba yatasaidia.Ndugu Wananchi,Katika kutafakari kipindi cha mwaka wa kwanza, wa Awamu ya Saba, ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, napenda nikiri kuwa changamoto kadhaa zilijitokeza zikiwemo zile zinazohusiana na masuala ya kiutendaji na kazi zetu za kila siku Serikalini. Tutajitahidi tuzipatie ufumbuzi changamoto hizo ili hatimae ziwe na mafanikio.Katika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo tutahakikisha kwamba Sheria Nam. 2 ya Utumishi wa Umma, inatumika kikamilifu kwa watumishi wa Serikali. Nawasihi watumishi wote wa umma wabadilike kwa kufuata misingi ya kujituma, kuheshimu maadili, kuzingatia sheria ziliopo na kuweka mbele utoaji wa huduma kwa wananchi panapostahiki bila ya ubaguzi, dharau au bughudha.Ndugu Wananchi,Jambo kubwa na la msingi tunalopaswa kulienzi na kuliendeleza kwa bidii zetu zote ni suala zima la umoja na mshikamano wetu ambao ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo yetu.Wito wangu kwenu ni kuzidi kuimarisha umoja na mshikamano wetu ambao umeleta amani na utulivu na mafanikio tuliyoyapata. Napenda kuchukua fursa hii kukupongezeni viongozi na wananchi nyote kwa msimamo wenu imara wa kudumisha umoja wetu tukitilia maanani kuwa “umoja ni nguvu’.Ndugu Wananchi,Wakati tumo katika harakati za kujiletea maendeleo yetu hapo tarehe 10 Septemba, 2011, tulipatwa na msiba mkubwa kwa kuondokewa na wananchi wenzetu waliotangulia mbele ya haki, wengine kuumia na kupoteza mali zao; kutokana na kuzama kwa meli ya “MV Spice Islander I” katika eneo la Nungwi, ilipokuwa ikielekea katika kisiwa cha Pemba.Baada ya tukio hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliunda Tume ya kuchunguza mazingira yaliyopelekea kutokea kwa ajali hio. Nachukua fursa hii kukujuilisheni kwamba tume hiyo imeshamaliza kazi yake na imenikabidhi ripoti ya kazi yao siku ya tarehe 5 Novemba, 2011. Serikali imeanza kuifanyia kazi ripoti hio na taarifa rasmi itatolewa kwa wananchi hapo baadae.Kwa mara nyengine tena natoa pongezi kwa makamanda na wapiganaji wa vikosi vyote, madaktari, wauguzi, wananchi wote pamoja na Washirika wetu wa Maendeleo, viongozi mbali mbali wa nchi za nje na wananchi wao kwa jumla, kwa ushirikiano wao mkubwa na juhudi za pamoja walizofanya wakati wa maafa hayo. Shukurani nyingi ziende kwa vyombo mbali mbali vya habari na watendaji wake kwa namna walivyokuwa wakiwapa taarifa wananchi juu ya matukio mbali mbali ya ajali hiyo. Moyo wa umoja na mshikamano wa Wazanzibari na ndugu zetu wa Tanzania Bara uliendelezwa kwa dhati katika kipindi hicho kigumu ulinivutia sana na tuna kila sababu ya kuuendeleza, wakati wote. Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki na aziweke roho zao mahali pema peponi – Amin.Ndugu Wananchi,Kadhalika, nachukua fursa hii, natoa shukurani za pekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kushirikiana nasi wakati wote na kwa kusimamia imara, kuudumisha na kuuendeleza muungano wetu na kwamba wakati wote yupo tayari kuzikabili changamoto za muungano wetu na kuzizungumza kwa uwazi pamoja na kutafuta njia ya kuzitatua. Pia, natoa shukurani kwa Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Gharib Mohamed Bilal, kwa kushirikiana na kwa kuendelea kuisimamia kamati ya pamoja ya SMT na SMZ ya kujadili masuala ya muungano.Shukurani zangu za dhati zimwendee Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, wakiwa washauri na wasaidizi wangu wakuu kwa kazi kubwa wanayoifanya. Ushauri wao kwangu na jitihada zao umetuwezesha sote kwa pamoja kutekeleza wajibu wetu wa kuwatumikia wananchi ipasavyo. Nyote ni mashahidi ya hilo. Aidha, natoa shukurani kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Masheha na Viongozi wote wa Zanzibar kwa kuendelea kufanyakazi kwa bidii katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Kadhalika, nachukua fursa hii kuzipongeza nchi marafiki na washirika wetu wa maendeleo ambao siku zote wamekuwa wakishirikiana nasi katika jitihada za kuiletea maendeleo nchi yetu. Nia yangu ni kuimarisha uhusiano huu mkubwa uliopo ili kwa pamoja tuweze kuiletea maendeleo zaidi Zanzibar. Pia, natoa shukurani nyingi kwa waandishi na vyombo vya habari kwa ushirikiano mzuri waliotupa katika kuielimisha jamii juu ya matukio mbali mbali nchini mwetu. Kwa namna ya pekee nawashukuru wananchi wote Watanzania kwa mashirikiano yao makubwa na Serikali zetu zote mbili.Shukurani maalum ziwaendee wananchi wote wa Zanzibar kwa mshikamano wao na moyo wao wa kujituma katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Mafanikio tulionayo, hapana shaka yametokana na juhudi zao.Kwa kumalizia nachukua fursa hii kwa aina ya pekee kuipongeza Kamati ya Maandalizi na Maadhimisho ya Kutimiza Miaka 48 ya Mapinduzi na Kamati zake zote kwa matayarisho mazuri ya Sherehe zetu hizi ambazo zimefana sana. Navishukuru vikosi vyote vilivyoshiriki gwaride pamoja na wananchi na wanafunzi wote walioshiriki maandamano ya leo ambayo ni ya kupigiwa mfano.Ahsanteni kwa kunisikiliza.MAPINDUZI DAIMAMungu Ibariki ZanzibarMungu Ibariki TanzaniaMungu Ibariki Afrika ................
................

In order to avoid copyright disputes, this page is only a partial summary.

Google Online Preview   Download